9. Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua.
10. Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.
11. Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.
12. Maana mwanadamu naye hajui wakati wake; kama samaki wanaokamatwa katika nyavu mbaya, na mfano wa ndege wanaonaswa mtegoni, kadhalika wanadamu hunaswa katika wakati mbaya, unapowaangukia kwa ghafula.
13. Pia nimeona hekima chini ya jua, nayo ni kama hivi, tena kwangu mimi ilionekana kuwa ni neno kubwa.
14. Palikuwa na mji mdogo, na watu ndani yake walikuwa wachache; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga.
15. Basi, kulionekana humo mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu ye yote aliyemkumbuka yule mtu maskini.
16. Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi.
17. Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa,Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu.
18. Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita;Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi.