Mdo 28:21-29 Swahili Union Version (SUV)

21. Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Uyahudi, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako.

22. Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana katika habari za madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali.

23. Wakiisha kuagana naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza kwa taratibu na kuushuhudia ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni.

24. Wengine waliamini yale yaliyonenwa, wengine hawakuyaamini.

25. Na walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha nabii Isaya,

26. akisema,Enenda kwa watu hawa, ukawaambie,Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu;Na kuona, mtaona wala hamtatambua;

27. Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa,Na masikio yao ni mazito ya kusikia,Na macho yao wameyafumba;Wasije wakaona kwa macho yao,Na kusikia kwa masikio yao,Na kufahamu kwa mioyo yao,Na kubadili nia zao, nikawaponya.

28. Basi ijulikane kwenu ya kwamba wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwa Mataifa, nao watasikia! [

29. Alipokwisha kusema hayo, Wayahudi wakaenda zao, wakiulizana mengi wao kwa wao.]

Mdo 28