Mdo 19:32-41 Swahili Union Version (SUV)

32. Basi wengine walikuwa wakilia hivi na wengine hivi; kwa maana ule mkutano ulikuwa umechafuka-chafuka, na wengi wao hawakuijua sababu ya kukusanyika kwao pamoja.

33. Wakamtoa Iskanda katika mkutano, Wayahudi wakimweka mbele ya watu. Iskanda akawapungia mkono, akitaka kujitetea mbele ya wale watu.

34. Lakini walipotambua ya kuwa yeye ni Myahudi, wakapiga kelele wote pia kwa sauti moja kwa muda wa kama saa mbili, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu.

35. Na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, Enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi, aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni?

36. Basi kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, imewapasa kutulia; msifanye neno la haraka haraka.

37. Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana mungu mke wetu.

38. Basi ikiwa Demetrio na mafundi walio pamoja naye wana neno juu ya mtu, baraza ziko, na maliwali wako; na washitakiane.

39. Bali mkitafuta neno lo lote katika mambo mengine, yatatengenezwa katika kusanyiko lililo halali.

40. Kwa maana tuna hatari ya kushitakiwa kwa ajili ya matata haya ya leo, ambayo hayana sababu; na katika neno hilo, hatutaweza kujiudhuru kwa mkutano huu.

41. Alipokwisha kusema haya akauvunja mkutano.

Mdo 19