Lk. 5:9-24 Swahili Union Version (SUV)

9. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata;

10. na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.

11. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.

12. Ikawa, alipokuwa katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma; naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.

13. Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukamwondoka.

14. Akamkataza asimwambie mtu, ila, Nenda ukajionyeshe kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao.

15. Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao.

16. Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.

17. Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya.

18. Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake.

19. Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu.

20. Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako.

21. Basi, wale waandishi na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wakisema, Ni nani huyu asemaye maneno ya kukufuru? N’nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?

22. Na Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnahojiana nini mioyoni mwenu?

23. Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende?

24. Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako.

Lk. 5