1. Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.
2. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?
3. Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.
4. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?
5. Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.
6. Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.
7. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?
8. Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi;
9. nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.
10. Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo.
11. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa.
12. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.
13. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.