Lk. 12:43-54 Swahili Union Version (SUV)

43. Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo.

44. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote.

45. Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa;

46. bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini.

47. Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.

49. Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?

50. Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!

51. Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano.

52. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu.

53. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.

54. Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.

Lk. 12