Kut. 9:4-18 Swahili Union Version (SUV)

4. Kisha BWANA atawatenga wanyama wa Israeli na wanyama wa Misri; wala hakitakufa kitu cho chote cha wana wa Israeli.

5. Naye BWANA akaweka muda, akasema, Kesho BWANA atalifanya jambo hili katika nchi.

6. BWANA akalifanya jambo hilo siku ya pili, na wanyama wote wa kufugwa wa Misri wakafa; lakini katika wanyama wa wana wa Israeli hakufa hata mmoja.

7. Farao akatuma watu, na tazama, hapana mmoja aliyekufa katika wanyama wa wana wa Israeli. Lakini moyo wa Farao ulikuwa mzito, wala hakuwapa hao watu ruhusa waende zao.

8. BWANA akawaambia Musa na Haruni, Jitwalieni konzi za majivu ya tanuuni, kisha Musa na ayarushe juu kuelekea mbinguni mbele ya Farao.

9. Nayo yatakuwa ni mavumbi membamba juu ya nchi yote ya Misri, nayo yatakuwa majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama, katika nchi yote ya Misri.

10. Basi wakatwaa majivu ya tanuuni, na kusimama mbele ya Farao; na Musa akayarusha juu mbinguni nayo yakawa ni majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama.

11. Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya hayo majipu, kwa maana hao waganga walikuwa na majipu, na Wamisri wote walikuwa nayo.

12. BWANA akaufanya mgumu moyo wa Farao, asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyomwambia Musa.

13. BWANA akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie.

14. Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni mwote.

15. Kwa kuwa wakati huu ningekwisha kuunyosha mkono wangu, na kukupiga wewe na watu wako, kwa tauni, nawe ungekatiliwa mbali na kuondolewa katika nchi;

16. lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote.

17. Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao?

18. Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa.

Kut. 9