24. Nawe utie hiyo mikufu miwili ya dhahabu iliyosokotwa katika zile pete mbili zilizo katika ncha za kifuko cha kifuani.
25. Na ncha zile nyingine za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa utazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera upande wa mbele.
26. Nawe utafanya pete mbili za dhahabu, uzitie katika hizo ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani.
27. Nawe fanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya mabegani vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.
28. Nao watakikaza kile kileso kwa zile pete zake kwenye pete za naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kwamba kikae pale juu ya ule mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, ili kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera.
29. Na Haruni atayachukua majina ya wana wa Israeli katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu juu ya moyo wake, hapo atakapoingia ndani ya mahali patakatifu, kuwa ukumbusho mbele ya BWANA daima.
30. Nawe utie hizo Urimu na Thumimu katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu; nazo zitakuwa juu ya moyo wa Haruni, hapo atakapoingia ndani mbele ya BWANA; na Haruni atachukua hukumu ya hao wana wa Israeli juu ya moyo wake mbele ya BWANA daima.
31. Nawe fanya hiyo joho ya naivera ya rangi ya samawi yote.
32. Nayo itakuwa na tundu katikati yake kwa kupitisha kichwa; itakuwa na utepe wa kazi ya kusokotwa kuzunguka hilo tundu lake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, ili lisipasuke.
33. Nawe katika pindo zake utatia makomamanga ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, kuzunguka pindo zake kotekote; na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga pande zote;
34. njuga ya dhahabu na komamanga, njuga ya dhahabu na komamanga, katika pindo za joho kuizunguka pande zote.
35. Nayo itakuwa juu ya Haruni akitumika; na sauti ya hizo njuga itasikilikana hapo aingiapo ndani ya mahali patakatifu mbele ya BWANA na hapo atokapo nje, ili kwamba asife.
36. Nawe fanya bamba la dhahabu safi na kuchora juu yake, mfano wa machoro ya muhuri, MTAKATIFU KWA BWANA.