6. Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake.
7. Jitenge mbali na neno uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu.
8. Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.
9. Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
10. Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kuyavuna maongeo yake;
11. lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni.
12. Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng’ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.
13. Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako.
14. Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu.
15. Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu;
16. tena, sikukuu ya mavuno, hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya, mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani.
17. Mara tatu katika mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU.
18. Usisongeze damu ya dhabihu zangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala mafuta ya sikukuu yangu usiyaache kusalia hata asubuhi.
19. Ya kwanza ya malimbuko ya nchi yako utayaleta na kuyatia ndani ya nyumba ya BWANA, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
20. Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.
21. Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake.
22. Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao.
23. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali.