1. Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi BWANA alivyowaleta Israeli watoke Misri.
2. Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha,
3. pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi ya ugenini;
4. na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao.
5. Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepanga, kwenye mlima wa Mungu;
6. naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye.
7. Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani.
8. Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote BWANA aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi BWANA alivyowaokoa.
9. Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote BWANA aliowatendea Israeli, kwa alivyo waokoa mikononi mwa Wamisri.
10. Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe BWANA aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri.
11. Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.
12. Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu.
13. Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni.
14. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni?
15. Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu;
16. wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake.
17. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema.