23. Na wale Wamisri wakawafuatia, wakaingia ndani kati ya bahari, farasi zote za Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake.
24. Ikawa katika zamu ya alfajiri, BWANA akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri.
25. Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa BWANA anawapigania, kinyume cha Wamisri.
26. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao.
27. Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na BWANA akawakukutia mbali hao Wamisri kati ya bahari.
28. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja.
29. Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji yalikuwa ni kuta upande wao wa kuume, na upande wao wa kushoto.
30. Ndivyo BWANA alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni kwa bahari, wamekufa.
31. Israeli akaiona ile kazi kubwa aliyoifanya BWANA juu ya Wamisri, ndipo hao watu wakamcha BWANA, wakamwamini BWANA, na Musa mtumishi wake.