1. Tena itakuwa, mambo haya yote yatakapokujilia, baraka na laana nilizoweka mbele yako, nawe utakapozikumbuka kati ya mataifa yote, huko atakakokupeleka BWANA, Mungu wako,
2. nawe utakapomrudia BWANA, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;
3. ndipo BWANA, Mungu wako, atakapougeuza utumwa wako, naye atakuhurumia, tena atarejea na kukukusanya kutoka mataifa yote, huko alikokutawanyia BWANA, Mungu wako.
4. Watu wako waliotawanyika wakiwako katika ncha za mbingu za mwisho, kutoka huko atakukusanya BWANA, Mungu wako; kutoka huko atakutwaa;
5. atakuleta BWANA, Mungu wako, uingie nchi waliyomiliki baba zako, nawe utaimiliki; naye atakutendea mema, na kukufanya uwe watu wengi kuliko baba zako.
6. BWANA, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.