1. Pakiwa na mashindano kati ya watu, wakaenda maamuzini, na hao waamuzi wakawaamua; na wampe haki mwenye haki, na wamhukumie makosa yule mwovu;
2. na iwe, ikimpasa kupigwa yule mwovu, alazwe chini na mwamuzi, na kupigwa mbele ya uso wake, kwa kadiri ya uovu wake, kwa kuhesabu.
3. Aweza kumpiga fimbo arobaini asizidishe asije akaonekana nduguyo kuwa amedharauliwa kwako, azidishapo kwa kumpiga fimbo nyingi juu ya hizi.
4. Ng’ombe apurapo nafaka usimfunge kinywa.
5. Watakapoketi pamoja mtu na nduguye, mmojawapo akafa, wala hana mwana wa kiume, mke wa yule aliyekufa asiolewe nje na mgeni; nduguye yule mumewe amwingilie amweke kwake awe mkewe, kumfanyia yampasayo nduguye mumewe.
6. Na iwe, yule mzaliwa wa kwanza atakayemzaa, amfuate nduguye aliyekufa kwa jina lake, lisije likafutwa jina lake katika Israeli.
7. Na yule mtu kwamba hapendi kumtwaa mke wa nduguye, aende huyo mke wa nduguye langoni kwa wazee, akawaambie, Nduguye mume wangu yuakataa kumsimamishia nduguye jina katika Israeli, hataki kunitimizia yampasayo nduguye mume wangu.
8. Ndipo wamwite wazee wa mji wake waseme naye; naye akisimama na kusema, Sitaki mimi kumtwaa mwanamke huyu,
9. ndipo mke wa nduguye amkaribie mbele ya hao wazee, amvue kiatu chake mguuni mwake, na kumtemea mate ya uso; kisha atajibu yule mwanamke, aseme, Mume akataaye kumjengea nduguye nyumba yake na afanywe hivi.
10. Na jina lake katika Israeli liitwe, Nyumba ya mvuliwa kiatu.
11. Washindanapo waume wao kwa wao, akakaribia mke wa mmojawapo, ili kumwokoa mumewe katika mkono wa ampigaye, yule mke akatoa mkono wake, na kumkamata tupu yake;
12. umkate ule mkono wake, lisiwe na huruma jicho lako.