Kum. 2:1-14 Swahili Union Version (SUV)

1. Ndipo tukageuka, tukashika safari yetu kwenda jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu, kama alivyoniambia BWANA; tukawa kuizunguka milima ya Seiri siku nyingi.

2. BWANA akanena, akaniambia,

3. Mlivyouzunguka mlima huu vyatosha; geukeni upande wa kaskazini.

4. Nawe waagize watu, uwaambie, Mtapita kati ya mpaka wa ndugu zenu wana wa watu, uwaambie, Mtapita kati ya mpaka wa ndugu zenu wana wa Esau waketio Seiri; nao watawaogopa; basi jiangalieni nafsi zenu sana;

5. msitete nao; kwa maana sitawapa katika nchi yao kamwe, hata kiasi cha kukanyaga wayo wa mguu; kwa kuwa nimempa Esau milima ya Seiri kuwa milki yake.

6. Nunueni vyakula kwao kwa fedha, mpate kula; na maji nayo nunueni kwao kwa fedha, mpate kunywa.

7. Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, amekubarikia katika kazi yote ya mkono wako; amejua ulivyotembea katika jangwa kubwa hili; miaka arobaini hii alikuwa nawe BWANA, Mungu wako; hukukosa kitu.

8. Basi tukapita kando yao ndugu zetu wana wa Esau, waketio Seiri kutoka njia ya Araba, kutoka Elathi na kutoka Esion-geberi.Tukageuka tukapita njia ya bara ya Moabu.

9. BWANA akaniambia, usiwasumbue Wamoabi, wala usishindane nao katika mapigano; kwa kuwa sitakupa katika nchi yake kuimiliki; kwa sababu Ari nimewapa wana wa Lutu kuimiliki.

10. (Walioketi humo hapo kale ni Waemi, nao ni watu wakubwa, wengi, warefu, mfano wa Waanaki;

11. na hawa nao wadhaniwa kuwa majitu kama Waanaki; lakini Wamoabi huwaita Waemi.

12. Na Wahori nao walikuwa wakikaa Seiri hapo kale, lakini wana wa Esau waliwafuata; wakawaangamiza mbele yao, wakakaa badala yao; kama alivyofanya Israeli nchi ya milki yake aliyopewa na BWANA.)

13. Sasa basi ondokeni, mkakivuke kijito cha Zeredi. Nasi tukakivuka kile kijito cha Zeredi.

14. Na siku tulizokuwa tukienda kutoka Kadesh-barnea hata tulipovuka kijito cha Zeredi, zilikuwa ni miaka thelathini na minane; maana, hata walipokwisha kuangamizwa watu wa vita kutoka kati ya marago, kizazi chao chote, kama walivyoapiwa na BWANA.

Kum. 2