Kum. 17:11-20 Swahili Union Version (SUV)

11. kwa mfano wa sheria watakayokufunza, na kwa mfano wa hukumu watakayokuambia, fanya vivyo; usigeuke katika hukumu watakayokuonyesha, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto.

12. Na mtu afanyaye kwa kujikinai, kwa kutomsikiza kuhani asimamaye hapo kwa kumtumikia BWANA, Mungu wako, au mwamuzi, na afe mtu huyo; nawe utauondoa uovu katika Israeli.

13. Na hao watu wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena kwa kujikinai.

14. Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako ukaimiliki, na kukaa humo; nawe utakaposema, Nitaweka mfalme juu yangu mfano wa mataifa yote yaliyo kando-kando yangu;

15. usiache kumweka yule atakayechaguliwa na BWANA, Mungu wako, awe mfalme juu yako; umweke mmoja katika ndugu zako awe mfalme juu yako; usimtawaze mgeni juu yako, ambaye si ndugu yako.

16. Ila asifanye farasi wake kuwa wengi, wala asiwarudishe watu Misri, ili apate kufanya farasi kuwa wengi; kwa kuwa BWANA amewaambia, Tangu sasa msirudie tena njia ile.

17. Wala asijizidishie wake, ili moyo wake usikengeuke; wala asifanye fedha zake na dhahabu kuwa nyingi mno.

18. Tena na iwe, zamani aketipo juu ya kiti cha ufalme wake, ajiandikie nakala ya torati hii katika chuo, kufuata hicho kilicho mbele ya makuhani Walawi;

19. na awe nayo, asome humo siku zote atakazoishi; ili apate kujifunza kumcha BWANA, Mungu wake, ayashike maneno yote ya torati hii na amri hizi, kwa kuyafanya;

20. moyo wake usije ukainuliwa juu ya ndugu zake, wala asikengeuke katika maagizo, kwa mkono wa kuume wala wa kushoto; ili apate kuzifanya siku zake kuwa nyingi katika ufalme wake, yeye na wanawe, katikati ya Israeli.

Kum. 17