13. Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu.
14. Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa BWANA utajulikana, uwaelekeao watumishi wake, naye atawaonea adui zake ghadhabu.
15. Maana BWANA atakuja na moto, na magari yake ya vita kama upepo wa kisulisuli; ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto.
16. Kwa maana BWANA atateta na wote wenye mwili, kwa moto na kwa upanga wake; nao watakaouawa na BWANA watakuwa wengi.
17. Watu wale wajitakasao, na kujisafisha katika bustani, nyuma yake aliye katikati; wakila nyama ya nguruwe, na machukizo, na panya; watakoma pamoja, asema BWANA.
18. Nami nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu.
19. Nami nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, Tarshishi, na Puli, na Ludi, wavutao upinde, kwa Tubali na Yavani, visiwa vilivyo mbali; watu wasioisikia habari yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu wangu katika mataifa.
20. Nao watawaleta ndugu zenu wote kutoka mataifa yote, kuwa sadaka kwa BWANA, juu ya farasi, na katika magari, na katika machela, na juu ya nyumbu, na juu ya wanyama wepesi, mpaka mlima wangu mtakatifu Yerusalemu, asema BWANA; kama vile wana wa Israeli waletavyo sadaka yao nyumbani kwa BWANA katika chombo safi.
21. Na baadhi ya hao nitawatwaa kuwa makuhani na Walawi, asema BWANA.
22. Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele zangu, asema BWANA, ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa.
23. Na itakuwa, mwezi mpya hata mwezi mpya, na sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema BWANA.
24. Nao watatoka nje na kuitazama mizoga ya watu walioniasi; maana funza wao hatakufa, wala moto wao hautazimika nao watakuwa chukizo machoni pa wote wenye mwili.