4. Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, nami nitaistarehesha hukumu yangu iwe nuru ya mataifa.
5. Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu kabila za watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu.
6. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka.
7. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao.
8. Maana nondo itawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote.
9. Amka, amka, jivike nguvu,Ee mkono wa Bwana;Amka kama katika siku zile za kale,Katika vizazi vile vya zamani.
10. Si wewe uliyemkata-kata Rahabu?Uliyemchoma yule joka?Si wewe uliyeikausha bahari,Na maji ya vilindi vikuu;Uliyevifanya vilindi kuwa njia,Ili wapite watu waliokombolewa?
11. Nao waliokombolewa na BWANA watarejea,Watafika Sayuni, wakiimba;Furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao;Watapata shangwe na furaha;Huzuni na kuugua zitakimbia.