Isa. 43:13-24 Swahili Union Version (SUV)

13. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?

14. BWANA, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia.

15. Mimi ni BWANA, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu.

16. BWANA asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu;

17. atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi.

18. Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.

19. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.

20. Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu;

21. watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.

22. Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli.

23. Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani.

24. Hukuninunulia manukato kwa fedha, wala hukunishibisha kwa mafuta ya sadaka zako; bali umenitumikisha kwa dhambi zako, umenichosha kwa maovu yako.

Isa. 43