Isa. 41:15-25 Swahili Union Version (SUV)

15. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi.

16. Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.

17. Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, BWANA, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.

18. Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.

19. Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja;

20. ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa BWANA ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba.

21. Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.

22. Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; watuonyeshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye.

23. Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu; naam, tendeni mema au tendeni mabaya, ili tujipime, tukaone pamoja.

24. Tazameni, ninyi si kitu, tena kazi yenu si kitu; awachaguaye ninyi ni chukizo.

25. Nimemwinua mtu toka kaskazini, naye amekuja; toka maawio ya jua amekuja anitajaye jina langu; naye atawajilia maliwali kama akanyagaye matope, na kama mfinyanzi afinyangaye udongo.

Isa. 41