Isa. 2:10-19 Swahili Union Version (SUV)

10. Ingia ndani ya jabali; ukajifiche mavumbini mbele za utisho wa BWANA, mbele za utukufu wa enzi yake.

11. Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.

12. Kwa maana kutakuwa siku ya BWANA wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini.

13. Na juu ya mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani;

14. na juu ya milima mirefu yote, na juu ya vilima vyote vilivyoinuka;

15. na juu ya kila mnara mrefu, na juu ya kila ukuta ulio na boma;

16. na juu ya merikebu zote za Tarshishi, na juu ya kila taswira ipendezayo.

17. Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.

18. Nazo sanamu zitatoweka kabisa.

19. Na watu wataingia ndani ya pango za majabali, na ndani ya mashimo ya nchi, mbele za utisho wa BWANA na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia.

Isa. 2