Isa. 14:7-25 Swahili Union Version (SUV)

7. Dunia yote inastarehe na kutulia;Hata huanzilisha kuimba.

8. Naam, misunobari inakufurahia,Na mierezi ya Lebanoni, ikisema,Tokea wakati ulipolazwa chini wewe,Hapana mkata miti aliyetujia.

9. Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako,Ili kukulaki utakapokuja;Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako,Naam, walio wakuu wote wa dunia;Huwainua wafalme wote wa mataifa,Watoke katika viti vyao vya enzi.

10. Hao wote watajibu na kukuambia,Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi!Wewe nawe umekuwa kama sisi!

11. Fahari yako imeshushwa hata kuzimu,Na sauti ya vinanda vyako;Funza wametandazwa chini yako,Na vidudu vinakufunika.

12. Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi!Jinsi ulivyokatwa kabisa,Ewe uliyewaangusha mataifa!

13. Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni,Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu;Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano,Katika pande za mwisho za kaskazini.

14. Nitapaa kupita vimo vya mawingu,Nitafanana na yeye Aliye juu.

15. Lakini utashushwa mpaka kuzimu;Mpaka pande za mwisho za shimo.

16. Wao wakuonao watakukazia macho,Watakuangalia sana, wakisema,Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia,Huyu ndiye aliyetikisa falme;

17. Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake;Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?

18. Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima,Kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe;

19. Bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako,Kama chipukizi lililochukiza kabisa;Kama vazi la wale waliouawa,Wale waliochomwa kwa upanga,Wale washukao mpaka misingi ya shimo;Kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu.

20. Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi,Kwa maana umeiharibu nchi yako,Umewaua watu wako;Kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele.

21. Fanyeni tayari machinjo kwa watoto wake.Kwa sababu ya uovu wa baba zao;Wasije wakainuka na kuitamalaki nchi,Na kuujaza miji uso wa ulimwengu.

22. Nami nitainuka, nishindane nao; asema BWANA wa majeshi; na katika Babeli nitang’oa jina na mabaki, mwana na mjukuu; asema BWANA.

23. Tena nitaifanya hiyo nchi kuwa makao ya nungu, na maziwa ya maji; nami nitaifagilia mbali kwa ufagio wa uharibifu; asema BWANA wa majeshi.

24. BWANA wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa; na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea;

25. kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo nira yake iliyo juu yao itakapoondoka, na mzigo wake utatoka mabegani mwao.

Isa. 14