Hes. 23:5-23 Swahili Union Version (SUV)

5. BWANA akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya.

6. Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye.

7. Akatunga mithali yake, akasema,Balaki amenileta kutoka Aramu,Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki,Njoo! Unilaanie Yakobo,Njoo! Unishutumie Israeli.

8. Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani?Nimshutumuje, yeye ambaye BWANA hakumshutumu?

9. Kutoka kilele cha majabali namwona;Na kutoka milimani namtazama;Angalia, ni watu wakaao peke yao,Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa.

10. Ni nani awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo,Au kuhesabu robo ya Israeli?Na nife kifo chake mwenye haki,Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake.

11. Balaki akamwambia Balaamu, Umenitendea nini? Nimekuleta ili Uwalaani adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa kabisa.

12. Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile BWANA atialo kinywani mwangu?

13. Balaki akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao kutoka huko.

14. Akamchukua mpaka shamba la Sofimu, hata kilele cha Pisga, akajenga madhabahu saba, akatoa sadaka ng’ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.

15. Akamwambia Balaki, Simama hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami nitaonana na BWANA kule.

16. BWANA akaonana na Balaamu akatia neno kinywani mwake, akasema, Umrudie Balaki, ukaseme hivi.

17. Akafika kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu pamoja naye. Balaki akamwambia, BWANA amenena nini?

18. Naye akatunga mithali yake, akasema,Ondoka Balaki, ukasikilize;Nisikilize, Ee mwana wa Sipori;

19. Mungu si mtu, aseme uongo;Wala si mwanadamu, ajute;Iwapo amesema, hatalitenda?Iwapo amenena, hatalifikiliza?

20. Tazama, nimepewa amri kubariki,Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua.

21. Hakutazama uovu katika Yakobo,Wala hakuona ukaidi katika Israeli.BWANA, Mungu wake, yu pamoja naye,Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao.

22. Mungu amewaleta kutoka Misri,Naye ana nguvu kama nguvu za nyati.

23. Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo,Wala hapana uganga juu ya Israeli.Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa,Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!

Hes. 23