1. Sala ya nabii Habakuki.
2. Ee BWANA, nimesikia habari zako, nami naogopa;Ee BWANA, fufua kazi yako katikati ya miaka;Katikati ya miaka tangaza habari yake;Katika ghadhabu kumbuka rehema.
3. Mungu alikuja kutoka Temani,Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani.Utukufu wake ukazifunika mbingu,Nayo dunia ikajaa sifa yake.
4. Mwangaza wake ulikuwa kama nuru;Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake;Ndipo ulipofichwa uweza wake.
5. Mbele zake ilikwenda tauni,Na makaa ya moto yakatoka miguuni pake.
6. Akasimama, akaitetemesha dunia;Akatazama, akawasitusha mataifa;Na milima ya zamani ikatawanyika;Vilima vya kale vikainama;Miendo yake ilikuwa kama siku za kale.
7. Naliziona hema za Kushani katika taabu;Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka.
8. Je! BWANA aliikasirikia mito?Je! Hasira yako ilikuwa juu ya mito,Au ghadhabu yako juu ya bahari,Hata ukapanda farasi zako,Katika magari yako ya wokovu?