2. mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu,
3. mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi,
4. mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki,
5. mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, kuhani mkuu;
6. huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa BWANA, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa BWANA, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye.
7. Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta.
8. Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme.
9. Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye.
10. Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya BWANA, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli.
11. Basi hii ndiyo nakala ya waraka, mfalme Artashasta aliyompa Ezra, kuhani, mwandishi, naam, mwandishi wa maneno ya amri za BWANA, na wa sheria zake alizowapa Israeli.
12. Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, salamu kamili; wakadhalika.
13. Natoa amri ya kwamba wote walio wa watu wa Israeli, na makuhani wao, na Walawi, katika ufalme wangu, wenye nia ya kwenda Yerusalemu kwa hiari yao wenyewe, waende pamoja nawe.
14. Kwa kuwa umetumwa na mfalme, na washauri wake saba, ili kuuliza habari za Yuda na Yerusalemu, kwa sheria ya Mungu wako iliyo mkononi mwako;
15. na kuichukua fedha na dhahabu, ambayo mfalme, na washauri wake, kwa hiari yao, wamemtolea Mungu wa Israeli, akaaye Yerusalemu;