2. Na upana wa maingilio yake ulikuwa dhiraa kumi; na mbavu za maingilio zilikuwa dhiraa tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; akaupima urefu wake, dhiraa arobaini, na upana wake, dhiraa ishirini.
3. Kisha akaingia ndani, akapima kila mwimo wa maingilio, dhiraa mbili; nayo maingilio, dhiraa sita; na upana wa maingilio dhiraa saba.
4. Akaupima urefu wake; dhiraa ishirini, na upana wake, dhiraa ishirini, mbele ya hekalu; akaniambia, Hapa ndipo mahali patakatifu kuliko kila mahali.
5. Kisha akaupima ukuta wa nyumba, dhiraa sita; na upana wa kila chumba cha mbavuni, dhiraa nne, kuizunguka nyumba pande zote.
6. Na vile vyumba vya mbavuni vilikuwa na orofa tatu, moja juu ya mwenziwe; vilikuwa thelathini, safu baada ya safu; navyo viliingia ndani ya ukuta uliokuwa wa nyumba, kwa vile vyumba vya mbavuni pande zote vipate kushikamana nao, wala visishikamane na ukuta wa nyumba.
7. Na vile vyumba vya mbavuni vilizidi kuwa vipana, kwa kadiri vilivyoizunguka nyumba juu kwa juu; maana kule kuzunguka kwake kulikwenda juu kwa juu, kuizunguka nyumba; basi upana wa nyumba ulikuwa ule ule hata juu; basi hupanda juu toka chumba cha chini hata chumba cha juu, kwa njia ya kile chumba cha katikati.
8. Tena, nikaona ya kwamba nyumba ile ilikuwa na sakafu ya mawe, iliyoinuliwa pande zote; nayo misingi ya vyumba vya mbavuni ilikuwa mwanzi mzima wa dhiraa sita.
9. Unene wa ukuta uliokuwa wa vile vyumba vya mbavuni, upande wa nje, ulikuwa dhiraa tano; nayo nafasi iliyobaki ilikuwa dhiraa tano; na kati ya vyumba vya mbavuni vya nyumba,
10. na vyumba vya walinzi, upana wa dhiraa ishirini, kuizunguka nyumba pande zote.
11. Na milango ya vile vyumba vya mbavuni iliielekea nafasi ile iliyobaki, mlango mmoja ulielekea upande wa kaskazini, na mlango mmoja upande wa kusini; na upana wa nafasi iliyobaki ulikuwa dhiraa tano pande zote.
12. Nalo jengo lililokabili mahali palipotengeka upande wa magharibi, upana wake dhiraa sabini; na ukuta wa lile jengo, unene wake dhiraa tano pande zote, na urefu wake dhiraa tisini.