Eze. 28:8-24 Swahili Union Version (SUV)

8. Watakushusha hata shimoni; nawe utakufa kifo chao waliouawa kati ya bahari.

9. Je! Utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni Mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha.

10. Utakufa kifo cha hao wasiotahiriwa, kwa mikono ya wageni; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.

11. Tena neno la BWANA likanijia, kusema,

12. Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri.

13. Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.

14. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.

15. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.

16. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.

17. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.

18. Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao.

19. Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.

20. Neno la BWANA likanijia, kusema,

21. Mwanadamu, uuelekezee Sidoni uso wako, ukatabiri juu yake,

22. useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Sidoni, nami natukuzwa kati yako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetekeleza hukumu zangu ndani yake, na kutakasika ndani yake.

23. Maana nitampelekea tauni, na damu, katika njia kuu zake, na hao waliotiwa jeraha wataanguka kati yake, kwa upanga juu yake pande zote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

24. Wala hautakuwapo mchongoma uchomao kwa nyumba ya Israeli; wala mwiba uumizao miongoni mwa wote wamzungukao, waliowatenda mambo ya jeuri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

Eze. 28