Eze. 20:21-37 Swahili Union Version (SUV)

21. Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu, ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani.

22. Lakini naliuzuia mkono wangu, nikatenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao mbele ya macho yao naliwatoa.

23. Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali;

24. kwa sababu hawakuzitekeleza hukumu zangu, bali walizikataa amri zangu, nao walizitia unajisi sabato zangu, na macho yao yaliandama vinyago vya baba zao.

25. Tena naliwapa amri zisizokuwa njema, na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo;

26. nami nikawatia unajisi kwa matoleo yao wenyewe, kwa kuwa walipitisha motoni wote waliofungua tumbo; ili kuwafanya kuwa ukiwa, wakapate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

27. Basi, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Baba zenu wamenitukana kwa jambo hili, kwa kuwa wamekosa kosa juu yangu.

28. Kwa maana nilipokuwa nimekwisha kuwaingiza katika nchi ile, ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa, wakati huo walipoona kila mlima mrefu, na kila mti wenye majani mengi, walitoa matoleo yao huko, na huko walitoa chukizo la sadaka zao, na huko walifanya nukato la kupendeza, na huko walimimina sadaka zao za kunywewa.

29. Ndipo nikawauliza, Nini maana yake mahali palipoinuka mnapopaendea? Basi, jina lake mahali pale ni Bama hata leo.

30. Basi, uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mnajitia unajisi kwa kuzifuata njia za baba zenu? Mnakwenda kufanya uasherati kwa kuyafuata machukizo yao?

31. Tena mtoapo matoleo yenu, na kuwapitisha watoto wenu motoni, je! Mnajitia unajisi kwa vinyago vyenu vyote hata leo? Na mimi je! Niulizwe neno nanyi, Enyi nyumba ya Israeli? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi.

32. Na haya yote yaingiayo katika nia zenu hayatakuwa kamwe; ikiwa mmesema, Sisi tutakuwa sawasawa na mataifa, sawasawa na jamaa za nchi nyingine, kutumikia miti na mawe.

33. Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika, nitakuwa mfalme juu yenu;

34. nami nitawatoa katika mataifa, na kuwakusanya, na kuwatoa katika nchi mlizotawanyika ndani yake, kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika;

35. nami nitawaingiza katika jangwa la mataifa, na huko ndiko nitakakoteta nanyi uso kwa uso.

36. Kama nilivyoteta na baba zenu katika jangwa la Misri, ndivyo nitakavyoteta nanyi, asema Bwana MUNGU.

37. Nami nitawapitisha chini ya fimbo, nami nitawaingiza katika mafungo ya agano.

Eze. 20