1. Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2. Hapana shaka ninyi ndinyi watu halisi,Nanyi mtakapokufa, ndipo na hekima itakoma.
3. Lakini mimi pia, nina fahamu kama ninyi;Mimi si duni yenu ninyi;Naam, ni nani asiyejua mambo kama hayo?
4. Mimi ni mtu wa kuchekwa na jirani yake,Ni mtu niliyemwita Mungu, naye akanijibu;Huyo mwenye haki, aliye mtimilifu, amekuwa ni kicheko.
5. Katika mawazo yake huyo aliye na raha mna kudharau mashaka;Tayari kwa ajili ya wenye kuteleza miguu.
6. Hema za wapokonyi hufanikiwa,Na hao wamkasirishao Mungu hukaa salama;Mikononi mwao Mungu huleta vitu vingi.
7. Lakini sasa waulize hao wanyama, nao watakufundisha;Na nyuni wa angani, nao watakuambia;
8. Au nena na nchi, nayo itakufundisha;Nao samaki wa baharini watakutangazia.