25. Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Mtwae ng’ombe wa baba yako, yaani ng’ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo;
26. ukamjengee BWANA, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng’ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata.
27. Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama BWANA alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku.
28. Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng’ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa.
29. Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili.
30. Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo.
31. Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake.
32. Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake.
33. Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli.
34. Lakini roho ya BWANA ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata.
35. Kisha akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote; wao nao walikutana pamoja ili kumfuata; kisha akatuma wajumbe waende kwa Asheri, na kwa Zabuloni, na kwa Naftali; nao wakakwea ili kumlaki.
36. Gideoni akamwambia Mungu, Ikiwa wewe utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema,
37. tazama, nitaweka ngozi ya kondoo katika kiwanja cha kupuria; na kama ukiwapo umande juu ya ngozi tu, na nchi yote ikiwa kavu, basi, hapo ndipo nitakapojua ya kuwa utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.
38. Ikawa hivyo; kwa maana aliondoka asubuhi na mapema, akaikamua ile ngozi, akautoa ule umande katika ile ngozi, bakuli zima la maji.
39. Gideoni akamwambia Mungu, Hasira yako isiwake juu yangu, nami nitasema mara hii tu; nakuomba, nijaribu kwa ngozi hii mara hii tu; sasa ngozi tu na iwe kavu, na uwe umande juu ya nchi yote.