Amu. 4:17-24 Swahili Union Version (SUV)

17. Lakini Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi, Mkeni.

18. Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu, karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa bushuti.

19. Akamwambia, Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa, akamfunika.

20. Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana.

21. Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa.

22. Na tazama, Baraka alipokuwa akimfuatia Sisera; Yaeli akatoka ili kumlaki, akamwambia, Njoo, nami nitakuonyesha yule mtu unayemtafuta. Basi akamwendea, na tazama, Sisera amelala humo, amekufa, na hicho kigingi kilikuwa kipajini mwake.

23. Basi hivyo Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani mbele ya wana wa Israeli siku hiyo.

24. Mkono wa wana wa Israeli ukazidi kupata nguvu juu ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hata walipokuwa wamemwangamiza Yabini, mfalme wa Kanaani.

Amu. 4