8. Ila mfalme akawatwaa hao wana wawili wa Rispa, binti Aya, aliomzalia Sauli, Armoni na Mefiboshethi; na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliomzalia Adrieli, mwana wa Barzilai, Mmeholathi;
9. akawatia mikononi mwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele za BWANA, nao wakaangamia wote saba pamoja; wakauawa siku za mavuno, za kwanza, mwanzo wa mavuno ya shayiri.
10. Naye Rispa, binti Aya, akatwaa nguo ya magunia akajitandikia mwambani, tangu mwanzo wa mavuno hata waliponyeshewa mvua toka mbinguni; wala hakuacha ndege wa angani kukaa juu yao mchana, wala wanyama wa mwitu usiku.
11. Kisha akaambiwa Daudi hayo aliyoyafanya huyo Rispa binti Aya, suria wa Sauli.
12. Akaenda Daudi, akaitwaa mifupa ya Sauli na mifupa ya Yonathani mwanawe mikononi mwa watu wa Yabesh-gileadi; waliyoiiba katika njia ya Bethshani, hapo Wafilisti walipowatungika, katika siku hiyo waliyomwua Sauli huko Gilboa;
13. naye akaileta toka huko hiyo mifupa ya Sauli, na mifupa ya Yonathani mwanawe; nao wakaizoa mifupa yao waliotundikwa.
14. Kisha wakaizika mifupa ya Sauli na ya Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Zela, kaburini mwa Kishi babaye; wakafanya yote aliyoyaamuru mfalme. Na baadaye Mungu aliiridhia hiyo nchi.
15. Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israeli; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti; naye Daudi akaishiwa na nguvu.
16. Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai, ambaye uzito wa mkuki wake ulikuwa shekeli mia tatu za shaba kwa uzani, naye amejifungia upanga mpya, alijaribu kumwua Daudi.
17. Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti, akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israeli.
18. Ikawa baada ya hayo, kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai.