4. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, Uwakusanye pamoja kwangu kwa siku tatu watu wa Yuda, na uwepo wewe hapa.
5. Amasa akaenda kuwakusanya Yuda; lakini akakawia zaidi ya huo muda aliowekewa.
6. Basi Daudi akamwambia Abishai, Sasa Sheba, mwana wa Bikri, atatudhuru, kuliko Absalomu; twaa wewe watumishi wa bwana wako, ukamfuatie, asiingie katika miji yenye boma, na kujiponya machoni petu.
7. Ndipo wakatoka nyuma yake watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, na mashujaa wote; wakatoka Yerusalemu, ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri.
8. Basi walipokuwako kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Naye Yoabu alikuwa amefungwa mavazi yake ya vita aliyoyavaa, na juu yake alikuwa na mshipi, na upanga uliotiwa viunoni mwake ndani ya ala yake; naye alipokuwa akiendelea, ukaanguka.