28. Ahimaasi akainua sauti yake, akamwambia mfalme, Amani. Akainama mbele ya mfalme kifudifudi, akasema, Ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyewatoa watu hao walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme.
29. Mfalme akauliza, Je! Yule kijana, Absalomu, yu salama? Ahimaasi akajibu, Yoabu aliponituma mimi mtumishi wa mfalme, mimi mtumishi wako, naliona kishindo kikubwa, lakini sikujua sababu yake.
30. Naye mfalme akasema, Geuka, usimame hapa. Akageuka, akasimama.
31. Na tazama, yule Mkushi akafika; Mkushi akasema, Nina habari kwa bwana wangu mfalme; kwa maana BWANA amekulipizia kisasi leo juu ya hao wote walioinuka kupigana nawe.
32. Naye mfalme akamwambia yule Mkushi, Yule kijana, Absalomu, je! Yu salama? Yule Mkushi akajibu, Adui za bwana wangu mfalme, na wote wainukao ili kukudhuru, na wawe kama alivyo yule kijana.
33. Naye mfalme akataabika sana, akapanda juu, akaingia kile chumba kilichokuwa juu ya lango, akalia; na katika kwenda kwake alisema hivi, Mwanangu Absalomu! Ee mwanangu! Mwanangu Absalomu! Laiti ningalikufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu!