2 Sam. 17:13-25 Swahili Union Version (SUV)

13. Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake.

14. Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu.

15. Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha.

16. Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye.

17. Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini.

18. Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake.

19. Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lo lote.

20. Nao watumishi wa Absalomu wakamwendea yule mwanamke mle nyumbani; wakasema, Wako wapi Yonathani na Ahimaasi? Yule mwanamke akawaambia, Wamevuka kijito cha maji. Basi walipokwisha kuwatafuta wasiwaone, wakarudi Yerusalemu.

21. Kisha ikawa, baada ya kuondoka kwao, wale wakatoka kisimani, wakaenda wakamwarifu mfalme Daudi; wakamwambia Daudi, Ondokeni, mkavuke maji haya upesi; maana ndivyo alivyotoa shauri Ahithofeli juu yenu.

22. Ndipo Daudi, na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakaondoka, wakavuka Yordani; na kulipopambazuka hakubaki mmojawapo wao asiyevuka Yordani.

23. Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajisonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye.

24. Basi Daudi akaja Mahanaimu. Naye Absalomu akauvuka Yordani yeye na watu wote wa Israeli pamoja naye.

25. Naye Absalomu akamweka Amasa awe juu ya jeshi mahali pa Yoabu. Basi huyo Amasa alikuwa mwana wa mtu, jina lake Yetheri, Mwishmaeli, aliyeingia kwa Abigali, binti Nahashi, nduguye Seruya, mamaye Yoabu.

2 Sam. 17