2 Sam. 14:21-33 Swahili Union Version (SUV)

21. Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu.

22. Naye Yoabu akaanguka kifulifuli hata nchi, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumwa wake haja yake.

23. Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu.

24. Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme.

25. Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake.

26. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme.

27. Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso.

28. Absalomu akakaa miaka miwili mizima katika Yerusalemu; asimwone uso mfalme.

29. Ndipo Absalomu akatuma kumwita Yoabu, ampeleke kwa mfalme, lakini yeye akakataa kumjia; akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kuja.

30. Kwa hiyo akawaambia watumishi wake, Tazameni, shamba la Yoabu liko karibu na shamba langu, naye ana shayiri huko; nendeni mkalitie moto. Basi watumishi wa Absalomu wakalitia moto lile shamba.

31. Ndipo akaondoka Yoabu, akamwendea Absalomu nyumbani kwake, akamwambia, Kwa nini watumishi wako wamelitia moto shamba langu?

32. Absalomu akamjibu Yoabu, Angalia, nilituma kwako, kusema, Njoo kwangu, ili nikupeleke kwa mfalme kunena, Mbona nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningekuwako huko hata sasa; basi sasa na nimtazame uso mfalme; na ukiwapo uovu kwangu, na aniue.

33. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akamwambia hayo, naye alipomwita Absalomu, yeye akaja kwa mfalme, akainama kifulifuli hata nchi mbele ya mfalme; naye mfalme akambusu Absalomu.

2 Sam. 14