1. Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda.
2. Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote.
3. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki, jina lake Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi; naye Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana.
4. Naye akamwambia, Kwa nini, Ee mwana wa mfalme, unakonda hivi siku kwa siku? Hutaki kuniambia? Amnoni akamwambia, Nampenda Tamari, umbu la ndugu yangu, Absalomu.
5. Yonadabu akamwambia, Lala kitandani mwako ujifanye mgonjwa na babako atakapokuja kukutazama, umwambie, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile, akaandae chakula machoni pangu nikione, nikakile mkononi mwake.