27. basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; uwafundishapo njia njema iwapasayo waiendee; ukainyeshee mvua nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi.
28. Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao, au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote;
29. yo yote atakayoyaomba na kusihi mtu awaye yote, au watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu pigo lake mwenyewe, na msiba wake mwenyewe, akiinyoshea mikono nyumba hii;
30. basi usikie huko mbinguni, ukaapo, ukasamehe, ukampatilize kila mtu kwa kadiri ya njia zake zote; wewe umjuaye moyo; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu);
31. ili wakuche wewe, waziendee njia zako, siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
32. Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyoshwa; hao watakapokuja na kuomba wakiielekea nyumba hii;
33. basi usikie huko mbinguni, toka makaoni mwako, ukatende yote atakayokuomba huyo mgeni; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe, kama watu wako Israeli, tena wajue ya kuwa nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa jina lako.
34. Ikiwa watu wako wametoka kupigana na adui zao, utakakowatuma ko kote, wakikuomba kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
35. basi uyasikie huko mbinguni wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao.
36. Wakikukosa, (maana hakuna mtu asiyekosa), hata uwakasirikie, na kuwatia mikononi mwa adui zao, wawahamishe, na kuwachukua mateka mpaka nchi iliyo mbali au iliyo karibu;
37. basi wakikumbuka katika nchi walikohamishwa, na kutubu, na kukusihi katika nchi ya uhamisho wao, wakisema, Tumekosa, tumetenda kwa ukaidi, tumefanya maovu;
38. wakurudiapo kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya uhamisho wao, adui walikowahamisha, wakiomba na kuielekea nchi uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
39. basi uyasikie toka mbinguni, toka makaoni mwako, wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao; ukawasamehe watu wako, waliokosa juu yako.
40. Na sasa, Ee Mungu wangu, macho yako yafumbuke, nakusihi, masikio yako yakasikilize maombi yaombwayo mahali hapa.
41. Sasa, Ee BWANA, Mungu, uondoke, uende kwenye raha yako, wewe na sanduku la nguvu zako; makuhani wako, Ee BWANA, Mungu, wavikwe wokovu, watakatifu wako na washangilie mema.