19. Wakamnenea Mungu wa Yerusalemu, kana kwamba kuitaja miungu ya mataifa wa nchi, iliyo kazi ya mikono ya watu.
20. Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni.
21. Naye BWANA akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga.
22. Ndivyo BWANA alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.
23. Watu wengi walimletea BWANA zawadi huko Yerusalemu, na vitu vya thamani kwa Hezekia, mfalme wa Yuda; hata yeye akatukuka tangu wakati ule machoni pa mataifa yote.
24. Katika siku hizo Hezekia akaugua akawa katika hatari ya kufa; akamwomba BWANA; naye akasema naye, akampa ishara.
25. Walakini kadiri alivyofadhiliwa Hezekia hakumrudishia vivyo; kwa kuwa moyo wake ulitukuka; kwa hiyo ikawako hasira juu yake, na juu ya Yuda na Yerusalemu.
26. Hata hivyo Hezekia akajinyenyekeza kwa ajili ya huku kutukuka kwa moyo wake, yeye na wenyeji wa Yerusalemu, hata haikuwajia hasira ya BWANA siku za Hezekia.
27. Naye Hezekia akawa na mali nyingi mno na heshima; akajifanyizia hazina za fedha, na za dhahabu, na za vito, na za manukato, na za ngao, na za namna zote za vyombo vya thamani;
28. ghala pia za mazao ya nafaka na mvinyo na mafuta; na malisho ya wanyama wa namna zote, na makundi mazizini.
29. Tena akajifanyizia miji, na mali za kondoo na ng’ombe kwa wingi; maana Mungu alimtajirisha sana sana.
30. Naye huyo Hezekia ndiye aliyezuia chemchemi ya juu ya maji ya Gihoni, akayaleta chini moja kwa moja upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Akafanikiwa Hezekia katika kazi zake zote.