1. Basi hayo yote yalipokwisha, wakatoka Israeli wote waliokuwako waende miji ya Yuda, wakazivunja-vunja nguzo, wakayakata-kata maashera, wakabomoa mahali pa juu na madhabahu katika Yuda yote na Benyamini, katika Efraimu pia na Manase, hata walipokwisha kuviharibu vyote. Ndipo wana wa Israeli wote wakarudi, kila mtu kwa milki yake, mijini kwao.
2. Hezekia akaziweka zamu za makuhani na Walawi kwa zamu zao, kila mtu kwa kadiri ya huduma yake, makuhani na Walawi pia, kwa sadaka za kuteketezwa na kwa sadaka za amani, kutumika, na kushukuru, na kusifu, malangoni mwa matuo ya BWANA.
3. Tena akaweka sehemu ya mfalme ya mali zake kwa sadaka za kuteketezwa, yaani, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na sadaka za kuteketezwa za sabato, na za mwezi mpya, na sikukuu, kama ilivyoandikwa katika torati ya BWANA.
4. Tena akawaamuru watu waliokaa Yerusalemu, watoe sehemu ya makuhani na Walawi, ili hao wajibidiishe katika torati ya BWANA.