1. Hezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka ishirini na kenda; na jina la mamaye aliitwa Abiya binti Zekaria.
2. Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Daudi babaye.
3. Yeye, katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, katika mwezi wa kwanza, aliifungua milango ya nyumba ya BWANA, akaitengeneza.
4. Akawaingiza makuhani na Walawi, akawakusanya uwandani upande wa mashariki,
5. akawaambia, Nisikieni, enyi Walawi; jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba ya BWANA, Mungu wa baba zenu, mkautoe uchafu katika patakatifu.
6. Kwa maana baba zetu wameasi, na kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, Mungu wetu, wamemwacha, na kugeuzia mbali nyuso zao na makao ya BWANA, na kumpa maungo.
7. Tena wameifunga milango ya ukumbi, na kuzizima taa, wala hawakufukiza uvumba, wala hawakumtolea Mungu wa Israeli sadaka za kuteketezwa katika patakatifu.
8. Kwa hiyo hasira ya BWANA imekuwa juu ya Yuda na Yerusalemu, naye amewatoa kuwa matetemeko, wawe ushangao, na mazomeo, kama mwonavyo kwa macho yenu.
9. Kwa kuwa, tazama, baba zetu wameangamia kwa upanga, na wana wetu, na binti zetu, na wake zetu wametekwa kwa ajili ya hayo.
10. Basi nia yangu ni kufanya agano na BWANA, Mungu wa Israeli, ili kwamba hasira yake kali itugeukie mbali.
11. Basi wanangu, msijipurukushe sasa, kwa kuwa BWANA amewachagua ninyi msimame mbele yake, kumhudumia, nanyi mpate kuwa watumishi wake, mkafukize uvumba.
12. Ndipo wakaondoka Walawi, Mahathi mwana wa Amasai, na Yoeli mwana wa Azaria, wa wana wa Wakohathi; na wa wana wa Merari, Kishi mwana wa Abdi, na Azaria mwana wa Yehaleleli; na wa Wagershoni, Yoa mwana wa Zima na Edeni mwana wa Yoa;
13. na wa wana wa Elisafani, Shimri na Yeueli; na wa wana wa Asafu, Zekaria na Matania;