2 Nya. 23:10-20 Swahili Union Version (SUV)

10. Akawasimamisha watu wote, kila mtu mwenye silaha yake mkononi, toka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto, upande wa madhabahu na nyumba, kumzunguka mfalme pande zote.

11. Ndipo wakamleta nje mwana wa mfalme, wakamvika taji, na kumpa ule ushuhuda, wakamtawaza awe mfalme; Yehoyada na wanawe wakamtia mafuta, wakasema, Mfalme na aishi.

12. Na Athalia alipoisikia sauti ya watu, na ya walinzi, na ya hao waliomsifu mfalme, akaingia kwa watu nyumbani mwa BWANA;

13. akatazama, na angalia, mfalme amesimama karibu na nguzo yake mlangoni, nao maakida na wenye mapanda karibu na mfalme; wakafurahi watu wote wa nchi, wakapiga mapanda; waimbaji pia wakipiga vinanda, wakaongoza nyimbo za kusifu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akasema, Fitina! Fitina!

14. Yehoyada kuhani akawaleta nje maakida wa mamia, waliowekwa juu ya jeshi, akawaambia, Mtoeni nje kati ya safu; naye ye yote amfuataye, na auawe kwa upanga; kwani kuhani amesema, Msimwue katika nyumba ya BWANA.

15. Basi wakampisha njia; akaenda kwa kuingia pa mlango wa farasi nyumbani mwa mfalme; nao wakamwua huko.

16. Kisha, Yehoyada akafanya agano, yeye na watu wote, na mfalme, kwamba watakuwa watu wa BWANA.

17. Na watu wote wakaiendea nyumba ya Baali, wakaibomoa; wakavunja-vunja madhabahu zake na sanamu zake, wakamwua Matani kuhani wa Baali mbele ya madhabahu.

18. Yehoyada akauamuru usimamizi wa nyumba ya BWANA chini ya mkono wa makuhani Walawi, aliowagawa Daudi nyumbani mwa BWANA, ili wazisongeze sadaka za kuteketezwa za BWANA, kama ilivyoandikwa katika torati ya Musa, kwa kufurahi na kuimba, kama alivyoamuru Daudi.

19. Akawasimamisha walinzi malangoni pa nyumba ya BWANA, asiingie aliye mchafu kwa vyo vyote.

20. Akawatwaa maakida wa mamia, na watu wakubwa, na hao watawalao watu, na watu wote wa nchi, akamtelemsha mfalme kutoka nyumba ya BWANA; wakalipitia lango la juu waende nyumbani kwa mfalme, wakamketisha mfalme katika kiti cha ufalme.

2 Nya. 23