20. Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani?
21. Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo.
22. Basi sasa, angalia, BWANA ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye BWANA amenena mabaya juu yako.
23. Ndipo akakaribia Zedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu roho ya BWANA ili aseme na wewe?
24. Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.
25. Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme;
26. mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani.
27. Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.
28. Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-gileadi.
29. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha; nao wakaingia vitani.
30. Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru maakida wa magari yake, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.
31. Ikawa maakida wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Mfalme wa Israeli ni huyu. Basi wakamgeukia ili wapigane naye; lakini Yehoshafati akalia, na BWANA akamsaidia; Mungu akawafarakisha kwake.
32. Ikawa, maakida wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.
33. Na mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.
34. Pigano likazidi siku ile; lakini mfalme wa Israeli akajitegemeza garini juu ya Washami hata jioni; akafa kama wakati wa kuchwa kwa jua.