1. Ikawa ulipothibitika ufalme wa Rehoboamu, naye amepata nguvu, aliiacha torati ya BWANA, na Israeli wote pamoja naye.
2. Ikawa katika mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; kwa kuwa walikuwa wamemwasi BWANA;
3. mwenye magari elfu moja na mia mbili, na wapanda farasi sitini elfu; na watu wasiohesabika, waliotoka Misri pamoja naye; Walubi, na Wasukii, na Wakushi.
4. Akaitwaa miji yenye maboma iliyokuwa ya Yuda, akaja Yerusalemu.
5. Ndipo akaja Shemaya nabii kwa Rehoboamu, na kwa wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu kwa sababu ya Shishaki, akawaambia, BWANA asema hivi, Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo nami nimewaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.
6. Ndipo wakajinyenyekeza wakuu wa Israeli na mfalme; wakasema, BWANA ndiye mwenye haki.
7. Naye BWANA alipoona ya kwamba wamejinyenyekeza, neno la BWANA likamjia Shemaya, kusema, Wamejinyenyekeza; sitawaharibu; lakini nitawapa wokovu punde, wala ghadhabu yangu haitamwagika juu ya Yerusalemu kwa mkono wa Shishaki.
8. Walakini watamtumikia; ili wapate kujua utumwa wangu, na huo utumwa wa falme za nchi.
9. Basi Shishaki, mfalme wa Misri, akapanda juu ya Yerusalemu, akazichukua hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao za dhahabu alizozifanya Sulemani.
10. Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme.
11. Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa BWANA, wakaja walinzi wakazichukua, wakazirudisha tena chumbani mwa walinzi.
12. Naye alipojinyenyekeza, ghadhabu ya BWANA ikamgeukia mbali, asimharibu kabisa; tena yalionekana katika Yuda mambo mema.