2 Fal. 9:17-32 Swahili Union Version (SUV)

17. Basi mlinzi alikuwa anasimama juu ya mnara wa Yezreeli, akaliona lile kundi la watu wa Yehu, alipokuwa akija, akasema, Naona kundi la watu. Yoramu akasema, Haya! Mtwae mpanda farasi mmoja, ukampeleke aende kuwalaki, na kuwauliza, Je! Ni amani?

18. Basi mpanda farasi mmoja akatoka awalaki, akasema, Mfalme asema hivi, Je! Ni amani? Yehu akasema, Wewe una nini na amani? Geuka unifuate. Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Yule mjumbe amewafikilia, lakini harudi tena.

19. Ndipo akapeleka mpanda farasi wa pili, naye akawafikilia, akasema, Mfalme asema hivi, Je! Ni amani? Yehu akasema, Wewe una nini na amani? Geuka unifuate.

20. Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Amewafikilia wala harudi tena; na mwendo huu ni kama mwendo wa Yehu mwana wa Nimshi; maana analiendesha gari kwa kasi.

21. Yoramu akasema, Tandika gari. Wakalitandika gari lake. Yoramu mfalme wa Israeli akatoka, na Ahazia mfalme wa Yuda, kila mtu katika gari lake. Wakatoka ili kumlaki Yehu, wakamkuta katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli.

22. Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! Ni amani, Yehu? Akajibu, Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na uchawi wake ni mwingi?

23. Yoramu akageuza mikono yake, akakimbia, akamwambia Ahazia, Ni uhaini, Ahazia.

24. Yehu akavuta upinde wake kwa nguvu zake zote, akampiga Yoramu kati ya mikono yake, hata mshale ukamtoka penye moyo wake, akaanguka katika gari lake.

25. Ndipo Yehu akamwambia Bidkari, akida wake, Mtwae ukamtupe katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli; maana kumbuka, hapo mimi na wewe tulipokuwa tumepanda farasi zetu, na kumfuata Anabu baba yake, BWANA alimwekea mzigo huu, akasema;

26. Hakika, jana nimeiona damu ya Nabothi, na damu ya wanawe, asema BWANA; nami nitakulipa katika kiwanja hiki, asema BWANA. Basi sasa mtwae huyu ukamtupe katika kiwanja hicho, sawasawa na neno la BWANA.

27. Na Ahazia mfalme wa Yuda alipoona hayo, akakimbia kwa njia ya nyumba ya bustanini. Yehu akamfuatia, akasema, Mpigeni huyu naye katika gari lake; wakampiga hapo penye kupandia Guri, karibu na Ibleamu. Akakimbilia Megido, akafa huko.

28. Na watumishi wake wakamchukua garini mpaka Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake pamoja na baba zake katika mji wa Daudi.

29. Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda.

30. Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; akatia uwanja machoni mwake, akapamba kichwa chake, akachungulia dirishani.

31. Hata Yehu alipoingia lango la mji, alisema, Je! Ni amani, Ewe Zimri, mwenye kumwua bwana wako?

32. Akainua uso wake kulielekea dirisha, akasema, Aliye upande wangu ni nani? Matowashi wawili watatu wakachungulia.

2 Fal. 9