11. Ndipo Yehu akatoka akawaendea watumishi wa bwana wake. Mmoja wao akamwuliza, Je! Ni amani? Huyu mwenye wazimu amekujia kwa nini? Akawaambia, Ninyi mnamjua mtu huyu na habari ya maneno yake.
12. Wakasema, Ni uongo; haya, tuambie. Akasema, Aliniambia haya na haya, akisema, BWANA asema hivi, Nimekutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli.
13. Basi wakafanya haraka, kila mtu akalitwaa vazi lake, na kulitia chini yake juu ya madaraja, wakapiga baragumu wakasema, Yehu ni mfalme.
14. Hivyo Yehu, mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya fitina juu ya Yoramu.Basi Yoramu alikuwa akiulinda Ramoth-Gileadi, yeye na Israeli wote, kwa sababu ya Hazaeli mfalme wa Shamu.
15. Lakini mfalme Yoramu mwenyewe alikuwa amerudi, apate kupona jeraha zake alizotiwa na Washami, alipokuwa akipigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Yehu akasema, Kama hii ndiyo nia yenu, basi, msimwache hata mtu mmoja atoke mjini, ili aende kupeleka habari Yezreeli.
16. Basi Yehu akapanda gari lake kwenda Yezreeli; kwa maana Yoramu alikuwa amelala huko; na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameshuka ili kumtazama Yoramu.
17. Basi mlinzi alikuwa anasimama juu ya mnara wa Yezreeli, akaliona lile kundi la watu wa Yehu, alipokuwa akija, akasema, Naona kundi la watu. Yoramu akasema, Haya! Mtwae mpanda farasi mmoja, ukampeleke aende kuwalaki, na kuwauliza, Je! Ni amani?
18. Basi mpanda farasi mmoja akatoka awalaki, akasema, Mfalme asema hivi, Je! Ni amani? Yehu akasema, Wewe una nini na amani? Geuka unifuate. Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Yule mjumbe amewafikilia, lakini harudi tena.
19. Ndipo akapeleka mpanda farasi wa pili, naye akawafikilia, akasema, Mfalme asema hivi, Je! Ni amani? Yehu akasema, Wewe una nini na amani? Geuka unifuate.
20. Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Amewafikilia wala harudi tena; na mwendo huu ni kama mwendo wa Yehu mwana wa Nimshi; maana analiendesha gari kwa kasi.
21. Yoramu akasema, Tandika gari. Wakalitandika gari lake. Yoramu mfalme wa Israeli akatoka, na Ahazia mfalme wa Yuda, kila mtu katika gari lake. Wakatoka ili kumlaki Yehu, wakamkuta katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli.
22. Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! Ni amani, Yehu? Akajibu, Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na uchawi wake ni mwingi?
23. Yoramu akageuza mikono yake, akakimbia, akamwambia Ahazia, Ni uhaini, Ahazia.
24. Yehu akavuta upinde wake kwa nguvu zake zote, akampiga Yoramu kati ya mikono yake, hata mshale ukamtoka penye moyo wake, akaanguka katika gari lake.
25. Ndipo Yehu akamwambia Bidkari, akida wake, Mtwae ukamtupe katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli; maana kumbuka, hapo mimi na wewe tulipokuwa tumepanda farasi zetu, na kumfuata Anabu baba yake, BWANA alimwekea mzigo huu, akasema;
26. Hakika, jana nimeiona damu ya Nabothi, na damu ya wanawe, asema BWANA; nami nitakulipa katika kiwanja hiki, asema BWANA. Basi sasa mtwae huyu ukamtupe katika kiwanja hicho, sawasawa na neno la BWANA.
27. Na Ahazia mfalme wa Yuda alipoona hayo, akakimbia kwa njia ya nyumba ya bustanini. Yehu akamfuatia, akasema, Mpigeni huyu naye katika gari lake; wakampiga hapo penye kupandia Guri, karibu na Ibleamu. Akakimbilia Megido, akafa huko.
28. Na watumishi wake wakamchukua garini mpaka Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake pamoja na baba zake katika mji wa Daudi.
29. Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda.