3. Pamoja na hayo alishikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo kwa hizo aliwakosesha Israeli; wala hakuziacha.
4. Basi Mesha, mfalme wa Moabu, alikuwa mfuga kondoo; naye alikuwa akimlipa mfalme wa Israeli sufu ya wana-kondoo elfu mia, na ya kondoo waume elfu mia.
5. Lakini ikawa, Ahabu alipokufa, mfalme wa Moabu akamwasi mfalme wa Israeli.
6. Akatoka wakati ule ule mfalme Yoramu katika Samaria, akawahesabu Israeli wote.
7. Akaenda akatuma kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akasema, Mfalme wa Moabu ameniasi; je! Utakwenda pamoja nami tupigane na Moabu? Akasema, Nitakwenda; mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi zangu ni kama farasi zako.
8. Akauliza, Njia ipi tuiendee? Akajibu, Njia ya jangwa la Edomu.
9. Basi mfalme wa Israeli akaenda, na mfalme wa Yuda, na mfalme wa Edomu; wakazunguka mwendo wa siku saba; wala hapakuwa na maji kwa jeshi, wala kwa wanyama waliowafuata.
10. Mfalme wa Israeli akasema, Ole wetu! Kwani BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu.
11. Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hapana hapa nabii wa BWANA, ili tumwulize BWANA kwa yeye? Akajibu mtumishi mmoja wa mfalme wa Israeli, akasema, Yupo hapa Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akimimina maji juu ya mikono yake Eliya.
12. Yehoshafati akasema, Neno la BWANA analo huyu. Basi mfalme wa Israeli, na Yehoshafati, na mfalme wa Edomu, wakamshukia.
13. Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, Nina nini mimi nawe? Uende kwa manabii wa babayo, na manabii wa mamayo. Mfalme wa Israeli akamwambia, La, sivyo; kwa kuwa BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu.
14. Elisha akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe.
15. Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake.
16. Akasema, BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki.
17. Kwa kuwa BWANA asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng’ombe zenu, na wanyama wenu.