2 Fal. 10:23-36 Swahili Union Version (SUV)

23. Akaingia Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu nyumbani mwa Baali, akawaambia waliomwabudu Baali, Tafuteni mkaangalie, asiwepo hapa pamoja nanyi mtu amtumikiaye BWANA, ila wamwabuduo Baali peke yao.

24. Wakaingia ili watoe dhabihu na sadaka za kuteketezwa. Basi Yehu alikuwa amejiwekea nje watu themanini, akasema, Mtu mmoja akiokoka wa watu niliowatia mikononi mwenu, amwachaye huyo, roho yake itakuwa badala ya roho yake.

25. Ikawa mara alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa, Yehu akawaambia walinzi na maakida, Ingieni mwapige; mtu awaye yote asitoke. Basi wakawapiga kwa makali ya upanga; walinzi na maakida wakawatupa nje, wakaenda mpaka mji wa nyumba ya Baali.

26. Wakazitoa nguzo zilizokuwamo nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza.

27. Wakaibomoa nguzo ya Baali, na kuiangusha nyumba ya Baali, wakaifanya choo hata leo.

28. Ndivyo Yehu alivyomharibu Baali katika Israeli.

29. Walakini katika makosa yake Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, Yehu hakutoka katika kuyafuata, yaani, ndama za dhahabu zilizokuwako katika Betheli na Dani.

30. BWANA akamwambia Yehu, Kwa kuwa umetenda vema kwa kufanya vilivyo haki machoni pangu, kuitendea nyumba ya Ahabu sawasawa na yote yaliyomo moyoni mwangu, wana wako wa kizazi cha nne watakaa kitini mwa Israeli.

31. Lakini Yehu hakuangalia, aende katika sheria ya BWANA, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote; hakutoka katika makosa ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.

32. Siku zile BWANA akaanza kupunguza Israeli. Hazaeli akawapiga mipakani mwote mwa Israeli;

33. kutoka Yordani upande wa mashariki, nchi yote ya Gileadi, na ya Wagadi, na Wareubeni, na Wamanase, kutoka Aroeri iliopo karibu na bonde la Arnoni, yaani, Gileadi, na Bashani.

34. Basi mambo yote ya Yehu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

35. Yehu akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoahazi mwanawe akatawala mahali pake.

36. Na muda Yehu aliotawala juu ya Israeli katika Samaria ulikuwa miaka ishirini na minane.

2 Fal. 10