13. Yehu akakutana na ndugu za Ahazia mfalme wa Yuda, akawauliza, Ni nani ninyi? Wakamjibu, Sisi tu ndugu zake Ahazia; tunashuka kuwasalimu wana wa mfalme na wana wa malkia.
14. Akasema, Wakamateni wa hai. Wakawakamata wa hai, wakawaua penye birika ya nyumba ya kukatia manyoya kondoo, watu arobaini na wawili; wala hakumsaza mtu wao awaye yote.
15. Alipotoka huko akamkuta Yehonadabu mwana wa Rekabu akija kumlaki; akamsalimu akamwambia, Je! Moyo wako umenyoka, kama moyo wangu ulivyo pamoja na moyo wako? Akajibu Yehonadabu, Ndio. Yehu akamwambia, Kama ndio, nipe mkono wako. Akampa mkono, akamkalisha pamoja naye garini.
16. Akasema, Fuatana nami, ukaone wivu wangu kwa BWANA. Wakampandisha garini mwake.
17. Naye alipofika Samaria, aliwapiga wote waliomsalia Ahabu katika Samaria, hata akamwangamiza, sawasawa na neno la BWANA alilomwambia Eliya.
18. Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia, Ahabu alimtumikia Baali kidogo; bali Yehu atamtumikia sana.
19. Basi niitieni manabii wote wa Baali, wote wamwabuduo, na makuhani wake wote; mtu asikose kuwapo hata mmoja. Maana ninayo dhabihu kubwa ya kumtolea Baali; ye yote atakayekosa kuwapo hataishi. Lakini Yehu alifanya hayo kwa hila, ili awaharibu waliomwabudu Baali.
20. Yehu akasema, Takaseni kusanyiko la dini kwa Baali. Wakalitangaza.
21. Yehu akatuma wajumbe katika Israeli yote, nao wote waliomwabudu Baali wakaja, wala hakusalia mtu ye yote asiyekuja. Wakaingia nyumbani mwa Baali; ikajaa nyumba ya Baali tangu mlango hata mlango.
22. Akamwambia yule aliyekuwa juu ya hazina ya mavazi, Uwatolee mavazi wote wanaomwabudu Baali. Akawatolea mavazi.
23. Akaingia Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu nyumbani mwa Baali, akawaambia waliomwabudu Baali, Tafuteni mkaangalie, asiwepo hapa pamoja nanyi mtu amtumikiaye BWANA, ila wamwabuduo Baali peke yao.