1. Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Siklagi siku ya tatu, hao Waamaleki walikuwa wameshambulia Negebu, na Siklagi, nao wameupiga Siklagi, na kuuchoma moto;
2. nao wamewachukua mateka wanawake waliokuwamo wakubwa kwa wadogo; hawakuwaua wo wote, ila wakawachukua, wakaenda zao.
3. Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka.
4. Ndipo Daudi na watu waliokuwa pamoja naye wakainua sauti zao na kulia, hata walipokuwa hawana nguvu za kulia tena.
5. Na hao wake wawili wa Daudi walikuwa wamechukuliwa mateka, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, aliyekuwa mkewe Nabali, wa Karmeli.
6. Naye Daudi akafadhaika sana; kwa sababu watu walikuwa wakisema kwamba apigwe kwa mawe, kwa maana nafsi za hao watu wote walisononeka, kila mtu kwa ajili ya wanawe na binti zake; lakini Daudi alijitia nguvu katika BWANA, Mungu wake.
7. Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhali niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko.
8. Daudi akauliza kwa BWANA, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote.