1 Sam. 24:4-18 Swahili Union Version (SUV)

4. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia BWANA, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri.

5. Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli.

6. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.

7. Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaache kumwondokea Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake.

8. Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hata nchi, akamsujudia.

9. Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru?

10. Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.

11. Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata.

12. BWANA atuamue, mimi na wewe, na BWANA anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako.

13. Kama vile walivyosema watu wa kale katika mithali yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa juu yako.

14. Na mfalme wa Israeli ametoka ili kumfuatia nani? Unamwinda nani? Ni kuwinda mbwa mfu, au kiroboto.

15. Basi BWANA atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe na mkono wako.

16. Ikawa, Daudi alipokwisha kumwambia Sauli maneno hayo Sauli alisema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Naye Sauli akapaza sauti yake, akalia.

17. Akamwambia Daudi, Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda mabaya.

18. Nawe umeonyesha leo jinsi ulivyonitendea mema, kwani BWANA aliponitia mikononi mwako, hukuniua.

1 Sam. 24